Friday, May 18, 2012

[Photos] Mamia Ya Mashabiki Wa Simba Wamuaga Patrick Mafisango

 
Mchezaji wa Kimataifa wa Simba Marehemu Patrick Mafisango leo asubuhi ameagwa na mashabiki, Wanachama, wapenzi na wadau wa mpira wa miguu pamoja na tasnia nyingine mbali mbali za sanaa na burudani katika viwanja vya TCC Chang’ombe jijini Dar-Es-Salaam.
Mamia kwa mamia ya wapenzi na Wanachama wa timu hiyo ya Simba wakiongozwa na Mwenyekiti aliyepita MzeeHassan Dalali, Mwenyekiti wa sasa timu hiyo Mbunge wa Tabora mjini Ismail Aden Rage wameungana na viongozi wengine wa kitaifa akiwemo waziri wa habari, utamaduni na Michezo Mheshimiwa Fenelia Mkangala, Waziri Wa Afrika Mashariki Mh Samwel Sita, Mbunge wa Temeke Mh Abbas Mtemvu, Mwenyekiti wa kamati ya nidhamu TFF Bwana Alfred Tibaigana, Mwenyekiti wa klabu ya Yanga Lloyd Nchunga.
Aidha mandhari katika uwanja huo wa TCC Chang’ombe yalikuwa ya huzuni kubwa kwani baadhi ya wadau, wanachama na mashabiki pamoja na wachezaji mbali mbali wa timu za soka za Tanzania walibubujikwa na machozi wakati wakiutazama na kutoa heshima zao za mwisho hali iliyoongeza simanzi kwa waombolezaji.
Mchezaji Haruna Moshi Boban ndiye aliyeonekana kuumizwa zaidi na kifo cha mchezaji huyo ambaye alikuwa rafiki yake kipenzi na kushindwa kujizuia mara kwa mara pale alipoona watu wengine wakilia. Hali ilikuwa mbaya zaidi kwake pale alipoenda kutoa heshima zake za mwisho ilibidi ashikiliwe na mwenyekiti wa Klabu hiyo Mh Ismail Aden Rage.
Kwa ujumla tukio hilo la kutoa heshima na kuaga mwili wa Marehemu Mafisango lilienda vizuri ukuachilia matukio madogo madogo ya wananchi waliokuwa na taharuki ya kutaka kuwahi kuaga mwili huo wakijikuta wakipambana na askari polisi ambao walikuwepo wa kutosha na kudhibiti fujo ama matukio ya uvunjifu wa amani.
Bongo5 ilifanikiwa kuongea na ndugu wa karibu wa Marehemu Mafisango bwana Karemera Gaspas ambaye naye alikuwemo kwenye gari lilopata ajali na kusababisha kifo cha Mafisango ambaye alisema yeye alitoka na Mafisango pamoja na washikaji zao wawili na kwenda katika klabu ya usiku Maisha Club.
Tulijumuika na Bendi ya FM Academia kuanzia mida ya saa 4 usiku hadi majira ya saa 9 usiku. “ Patrick Mafisango alinipitia tukatoka pamoja na kwenda Club Maisha kuwaona FM Academia wakitumbuiza, sasa wakati tunarudi tukiwa maeneo ya Veta Changombe karibu kabisa na nyumbani kwa marehemu ilitokea Guta na Patrick alipojaribu kuikwepa gari ilimshinda na mimi nilikuja kushtuka tupo mtaroni na ndipo Mafisango alipofariki baada ya kupata majeraha mabaya usoni mwake na sehemu nyingine za mwili.
Kwa mujibu wa maelezo ya ratiba nzima ya mazishi mwili wa Patrick Mafisango unategemewa kusafirishwa kwa ndege leo jioni kuelekea jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo huku klabu ya Simba ikiwakilishwa na mjumbe wa kamati ya mashindano bwana Kinesi pamoja na mchezaji Haruna Moshi Boban ambaye alikuwa kipenzi chake. Mazishi yanategemewa kufanyika siku ya Jumapili huko huko Kinshasa nchini Congo.

No comments:

Post a Comment